Mathayo 9:18-38
Mathayo 9:18-38 NENO
Isa alipokuwa akiwaambia mambo haya, kiongozi wa sinagogi akaingia, akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” Isa akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye. Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Isa, akagusa upindo wa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Isa akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo. Isa alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote. Isa alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Isa akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.” Ndipo Isa akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” Macho yao yakafunguka. Isa akawaonya vikali, akisema, “Chungeni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote. Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Isa. Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea, na umati wa watu wakastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.” Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.” Isa akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri Habari Njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. Alipoona umati wa watu, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili atume watendakazi katika shamba lake la mavuno.”