Mathayo 8:23-33
Mathayo 8:23-33 NENO
Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. Ghafula, kukatokea dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Isa alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!” Naye Isa akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nayo bahari ikatulia kabisa. Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!” Walipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. Wakapaza sauti wakisema, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?” Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakila. Wale pepo wachafu wakamsihi Isa, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.” Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji. Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.