Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 5

5
Mahubiri ya Mlimani
(Mt 5–7)
1Basi Yesu alipoona makundi ya watu, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia.
Sifa za mtu aliyebarikiwa
(Lk 6:20‑23)
2Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:
3“Heri walio maskini wa roho,
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4Heri wale wanaohuzunika,
maana hao watafarijiwa.
5Heri walio wapole,
maana hao watairithi nchi.
6Heri wenye njaa na kiu ya haki,
maana hao watatoshelezwa.
7Heri wenye huruma,
maana hao watapata rehema.
8Heri walio na moyo safi,
maana hao watamwona Mungu.
9Heri walio wapatanishi,
maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11“Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena mabaya ya aina zote dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.
Chumvi na nuru
(Mk 9:50; Lk 14:34‑35)
13“Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliye ndani ya ile nyumba. 16Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Kutimiza Sheria
17“Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18Kwa maana, amin nawaambia, hadi mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwa Sheria, hadi kila kitu kiwe kimetimia. 19Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika ufalme wa mbinguni. 20Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.
Kuhusu hasira
(Lk 12:57‑59)
21“Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’#5:21 Kut 20:13 22Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka#5:22 neno la Kiaramu la dharau au dhihaka ya hali ya juu,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi#5:22 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa Jehanamu.
23“Kwa hiyo, ikiwa unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Nenda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
25“Patana na mshtaki wako upesi wakati mpo njiani kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26Amin, nakuambia, hutatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.
Kuhusu uzinzi
27“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’#5:27 Kut 20:14 28Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa Jehanamu. 30Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe Jehanamu.
Kuhusu talaka
(Mt 19:9; Mk 10:11‑12; Lk 16:18)
31“Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’#5:31 Kum 24:1 32Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.
Kuhusu kuapa
33“Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; 35au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.
Kuhusu kulipiza kisasi
(Lk 6:29‑30)
38“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’#5:38 Kut 21:24; Law 24:20; Kum 19:21 39Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40Mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41Mtu akikulazimisha kwenda maili moja#5:41 kama kilomita 1.6, nenda naye maili mbili#5:41 kama kilomita 3.2. 42Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.
Wapendeni adui zenu
(Lk 6:27‑28, 32‑36)
43“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’#5:43 Law 19:18 44Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu, na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47Nanyi mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu hawafanyi hivyo? 48Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia