Mathayo 5:27-48
Mathayo 5:27-48 NENO
“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa Jehanamu. Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe Jehanamu. “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini. “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Mwenyezi Mungu.’ Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. Mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. Mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu, na waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? Nanyi mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu hawafanyi hivyo? Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.