Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 28:1-10

Mathayo 28:1-10 NEN

Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi. Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu. Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ” Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 28:1-10