Mathayo 26
26
Kufa na kufufuka kwa Isa
(Mathayo 26–28)
Njama ya kumuua Isa
(Marko 14:1-2; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)
1Isa alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, 2“Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka#26:2 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri., naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”
3Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. 4Wakapanga kumkamata Isa kwa siri na kumuua. 5Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”
Isa apakwa mafuta huko Bethania
(Marko 14:3-9; Luka 7:35-38; Yohana 12:1-8)
6Isa alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. 7Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Isa alipokuwa ameketi mezani kula chakula.
8Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? 9Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”
10Isa, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. 11Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 12Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. 13Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
Yuda akubali kumsaliti Isa
(Marko 14:10-11; Luka 22:3-6)
14Kisha mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alienda kwa viongozi wa makuhani 15na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Isa mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Isa.
Isa ala Pasaka na wanafunzi wake
(Marko 14:12-21; Luka 22:7-23; Yohana 13:21-30)
17Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Isa wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
18Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19Hivyo wanafunzi wakafanya vile Isa alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.
20Ilipofika jioni, Isa alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 21Nao walipokuwa wakila, Isa akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
22Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”
23Isa akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. 24Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”
25Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Mwalimu?”
Isa akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”
Kuanzishwa kwa Chakula cha Bwana Isa
(Marko 14:22-26; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)
26Walipokuwa wanakula, Isa akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”
27Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba#26:29 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu.”
30Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
Isa atabiri kuwa Petro atamkana
(Marko 14:27-31; Luka 22:31-34; Yohana 13:31-38)
31Kisha Isa akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:
“ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’#26:31 Zekaria 13:7
32Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
33Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”
34Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
35Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Isa aomba katika Bustani ya Gethsemane
(Marko 14:32-42; Luka 22:39-46)
36Kisha Isa akaenda pamoja na wanafunzi wake hadi kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” 37Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38Kisha Isa akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”
39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”
40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”
43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.
45Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
Isa akamatwa
(Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yohana 18:1-11)
47Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49Mara Yuda akamjia Isa na kumsalimu, “Salamu, Mwalimu!” Akambusu.
50Isa akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”
Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Isa. 51Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Isa alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52Ndipo Isa akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
55Wakati huo, Isa akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Isa mbele ya Baraza la Wayahudi
(Marko 14:53-65; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)
57Wale waliomkamata Isa wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa Torati pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.
59Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi#26:59 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Isa ili wapate kumuua. 60Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.
Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo 61na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”
62Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Isa, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63Lakini Isa akakaa kimya.
Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Al-Masihi#26:63 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Mwana wa Mungu.”
64Isa akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
65Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia alivyokufuru. 66Uamuzi wenu ni gani?”
Wakajibu, “Anastahili kufa.”
67Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68na kusema, “Tutabirie, wewe Al-Masihi! Ni nani aliyekupiga?”
Petro amkana Isa
(Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)
69Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Isa wa Galilaya.”
70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”
71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Isa Al-Nasiri.”
72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”
73Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”
74Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”
Papo hapo jogoo akawika. 75Ndipo Petro akakumbuka lile neno Isa alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 26: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.