Mathayo 22
22
Mfano wa karamu ya arusi
(Luka 14:15-24)
1Isa akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, 2“Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.
4“Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’
5“Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. 6Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. 7Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.
8“Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. 9Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ 10Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.
11“Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. 12Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.
13“Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
14“Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”
Swali kuhusu kulipa kodi ya Kaisari
(Marko 12:13-17; Luka 20:20-26)
15Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Isa katika maneno yake. 16Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode#22:16 Wafuasi wa Mfalme Herode waliokubaliana na utawala wa Rumi. kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo. 17Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”
18Lakini Isa alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? 19Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. 20Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
21Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
Basi Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
22Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.
Ndoa wakati wa ufufuo
(Marko 12:18-27; Luka 20:27-40)
23Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Isa na kumuuliza swali, wakisema, 24“Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ 25Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. 26Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. 27Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. 28Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”
29Isa akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. 30Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 31Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, 32‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’#22:32 Kutoka 3:6? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”
33Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake.
Amri kuu kuliko zote
(Marko 12:28-34; Luka 10:25-28)
34Mafarisayo waliposikia kwamba Isa alikuwa amewanyamazisha Masadukayo#22:34 Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho., Mafarisayo wakakusanyika pamoja. 35Mmoja wao, mtaalamu wa Torati, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36“Mwalimu, ni amri ipi katika Torati iliyo kuu kuliko zote?”
37Isa akamjibu, “ ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’#22:37 Kumbukumbu 6:5 38Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’#22:39 Walawi 19:18 40Amri hizi mbili ndizo msingi wa Torati na Manabii.”
Al-Masihi ni Mwana wa nani?
(Marko 12:35-37; Luka 20:41-44)
41Mafarisayo wakiwa wamekusanyika pamoja, Isa akawauliza, 42“Mnaonaje kuhusu Al-Masihi#22:42 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.? Yeye ni mwana wa nani?”
Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
43Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, anamwita Al-Masihi ‘Bwana’? Kwa maana asema,
44“ ‘Mwenyezi Mungu alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.”#22:44 Zaburi 110:1’
45Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Isa neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 22: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.