Mathayo 22:34-46
Mathayo 22:34-46 NEN
Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.” Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.” Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema, “ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’ Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.