Mathayo 22:1-22
Mathayo 22:1-22 NENO
Isa akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja. “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’ “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto. “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni. “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema. “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’ “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.” Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Isa katika maneno yake. Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo. Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Isa alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Basi Isa akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.