Mathayo 21:1-9
Mathayo 21:1-9 NEN
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtamkuta punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Kama mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.” Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema: “Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mnyenyekevu, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ” Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani. Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema, “Hosana, Mwana wa Daudi!”