Mathayo 19:1-15
Mathayo 19:1-15 NENO
Isa alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Yudea, ng’ambo ya Yordani. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akawaponya huko. Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?” Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke, naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Wakamuuliza, “Kwa nini basi Musa aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?” Isa akawajibu, “Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!” Isa akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.” Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Isa ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta. Isa akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.