Mathayo 14:25-33
Mathayo 14:25-33 NEN
Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa. Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.” Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.” Yesu akamwambia, “Njoo.” Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!” Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”