Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13

13
Mfano wa mpanzi
(Marko 4:1-9; Luka 8:1-8)
1Siku hiyo hiyo Isa akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. 2Umati mkubwa mno wa watu wakakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. 3Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. 4Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. 6Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. 8Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. 9Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Sababu ya kufundisha kwa mifano
(Marko 4:10-12; Luka 8:9-10)
10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”
11Akawajibu, “Ninyi mmepewa ujuzi wa siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawajapewa. 12Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. 13Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano:
“Ingawa wanatazama, hawaoni;
wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi.
14Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema:
“ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa;
na pia mtatazama lakini hamtaona.
15Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu;
hawasikii kwa masikio yao,
na wamefumba macho yao.
Wasije wakaona kwa macho yao,
na wakasikiliza kwa masikio yao,
wakaelewa kwa mioyo yao,
na kugeuka nami nikawaponya.’#13:15 Isaya 6:9, 10
16Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. 17Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.
Maelezo ya mfano wa mbegu
(Marko 4:13-20; Luka 8:11-15)
18“Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: 19Mtu yeyote anaposikia neno la ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. 20Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na hulipokea mara moja kwa furaha. 21Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye anarudi nyuma mara moja. 22Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu anayelisikia neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. 23Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”
Mfano wa magugu
24Isa akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.
27“Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’
28“Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’
“Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’
29“Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo. 30Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”
Mfano wa punje ya haradali
(Marko 4:30-32; Luka 13:18-19)
31Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. 32Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”
Mfano wa chachu
(Luka 13:20-21)
33Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.”
34Isa alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. 35Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema:
“Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano;
nitahubiri mambo yaliyofichika
tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”#13:35 Zaburi 78:2
Ufafanuzi wa mfano wa magugu
36Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”
37Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. 38Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.
40“Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba#13:43 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.
Mfano wa hazina iliyofichwa na mfano wa lulu
44“Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.
45“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.
Mfano wa wavu
47“Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”
51Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”
Wakamjibu, “Ndiyo.”
52Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa Torati aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”
Isa akataliwa Nasiri
(Marko 6:1-6; Luka 4:16-30)
53Isa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. 54Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi#13:54 Nyumba ya ibada na mafunzo. lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza? 55Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” 57Wakachukizwa naye.
Lakini Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.”
58Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia