Mathayo 13:44-53
Mathayo 13:44-53 NENO
“Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua. “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.” Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakamjibu, “Ndiyo.” Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa Torati aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.” Isa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka.