Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:24-43

Mathayo 13:24-43 NENO

Isa akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ” Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.” Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.” Isa alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.” Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.