Mathayo 10:24-42
Mathayo 10:24-42 NENO
“Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake! “Basi msiwaogope, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinong’onwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika Jehanamu. Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi. “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. Kwa maana nimekuja kuleta uadui kati ya “ ‘mtu na baba yake, binti na mama yake, mkwe na mama mkwe wake; nao adui za mtu watakuwa ni wale watu wa nyumbani mwake.’ “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. “Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki. Mtu yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”