Luka 9:1-17
Luka 9:1-17 NENO
Yesu kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, kisha akawatuma waende wakahubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada. Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kungʼuteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.” Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali. Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu. Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka. Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ninayesikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona. Mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Kisha akaenda nao faraghani hadi mji uitwao Bethsaida. Lakini umati wa watu wakafahamu alikoenda, wakamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji. Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Yesu na kumwambia, “Waage watu hawa ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.” Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Nao wakajibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.” (Walikuwepo wanaume wapatao elfu tano.) Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika vikundi vya watu hamsini hamsini.” Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu. Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.