Luka 8:22-56
Luka 8:22-56 NENO
Siku moja Isa alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni hadi ng’ambo ya ziwa.” Nao wakaondoka. Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa. Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!” Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari. Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?” Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?” Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, iliyo upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya. Isa aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini. Alipomwona Isa, alipaza sauti, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!” Wakati huo Isa alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani. Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno. Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo. Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Isa awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu. Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama. Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani. Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Isa, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Isa, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa. Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa. Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Isa aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake. Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Isa afuatane naye, lakini Isa akamuaga, akamwambia: “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Isa alimtendea. Basi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu wakampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani mwake, kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na mbili, alikuwa anakufa. Isa alipokuwa akienda, umati wa watu wakamsonga sana. Palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, [na alikuwa amegharimia mali yake yote kwa matibabu] lakini hakuna yeyote aliyeweza kumponya. Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma. Isa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, umati huu wa watu wanakusonga na kukusukuma kila upande.” Lakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.” Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara moja. Basi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.” Isa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani mwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.” Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.” Walipofika nyumbani mwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yohana na Yakobo, pamoja na baba na mama wa yule binti. Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.” Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. Isa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote kuhusu yale yaliyotukia.