Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 6:27-49

Luka 6:27-49 NEN

“Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi. “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.” Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake. “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako. “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma. Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake. “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri. Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”