Luka 5:1-16
Luka 5:1-16 NENO
Siku moja Isa alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi walimsonga ili wapate kusikia neno la Mungu. Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua. Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama. Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni pa Isa na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia. Ndipo Isa akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” Hivyo wakasogeza mashua zao hadi ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata. Ikawa siku moja Isa alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Isa, alianguka chini hadi uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.” Isa akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika. Isa akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” Lakini habari zake Isa zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makundi makubwa ya watu walikuwa wakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Lakini mara kwa mara Isa alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.