Luka 24:36-53
Luka 24:36-53 NENO
Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Isa mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. Lakini Isa akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi mwenyewe. Niguseni mwone; kwa maana mzuka huna nyama na mifupa, kama mnavyoniona mimi.” Aliposema haya, akawaonesha mikono na miguu yake. Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, naye akakichukua na kukila mbele yao. Akawaambia, “Haya ndio yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu katika Torati ya Musa, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.” Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Haya ndio yaliyoandikwa: Al-Masihi atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. Ninyi ni mashahidi wa mambo haya. “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo kutoka juu.” Baada ya kuwaongoza hadi Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki. Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni. Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu.