Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:1-25

Luka 23:1-25 NENO

Kisha umati wote wa watu wakainuka na kumpeleka Isa kwa Pilato. Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita ni Al-Masihi, mfalme.” Basi Pilato akamuuliza Isa, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Isa akajibu, “Wewe wasema.” Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na umati ule wote, “Sioni msingi wowote wa kumshtaki mtu huyu!” Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Yudea yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!” Pilato aliposikia hayo akauliza kama huyo mtu alikuwa Mgalilaya. Alipofahamu kwamba Isa alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu. Herode alipomwona Isa alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha. Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Isa hakumjibu lolote. Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana. Herode na askari wake wakamdhihaki Isa na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato. Siku hiyo, Herode na Pilato wakapata urafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao. Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami sikupata msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. Wala Herode hakumpata na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachilia.” [ Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.] Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyu! Tufungulie Baraba!” (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.) Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena. Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.” Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda. Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe. Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.