Luka 22:7-19
Luka 22:7-19 NEN
Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.” Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?” Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia. Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.” Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka. Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.” Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.” Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”