Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 21:20-38

Luka 21:20-38 NENO

“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia. Wakati huo, wale walio Yudea wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walio mashambani wasiingie mjini. Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu. Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie. “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.” Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote. Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yakitukia, mtambue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia. “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama mtego unasavyo. Hivyo ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote wanaoishi katika uso wa dunia yote. Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.” Kila siku Isa alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alienda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha. Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.