Luka 20:20-26
Luka 20:20-26 NEN
Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki ili wapate kumtega kwa maneno asemayo, ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala. Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia, “Nionyesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni vya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya.