Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 2:1-20

Luka 2:1-20 NENO

Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi. (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.) Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa. Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nasiri ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito. Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia, naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ng’ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni. Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Mwenyezi Mungu akawatokea, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawang’aria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote. Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Al-Masihi, Bwana. Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ng’ombe.” Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Mwenyezi Mungu ametuambia habari zake.” Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ng’ombe. Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.