Luka 1:67-80
Luka 1:67-80 NENO
Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, naye akatoa unabii, akisema: “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa. Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake, (kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani), kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao: ili kuonesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka agano lake takatifu, kiapo alichomwapia baba yetu Ibrahimu: kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote. “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Mwenyezi Mungu na kuandaa njia kwa ajili yake, kuwajulisha watu wake wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao, kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru inayotoka juu itatuzukia ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.” Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionesha hadharani kwa Waisraeli.