Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 1:5-25

Luka 1:5-25 NENO

Wakati wa utawala wa Herode mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, aliyekuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Haruni. Zakaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana. Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zakaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba. Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zakaria. Zakaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina Yohana. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa Waisraeli warudi kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuwaweka tayari watu walioandaliwa kwa ajili ya Bwana.” Zakaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.” Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zakaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono. Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani mwake. Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano. Elizabeti akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponipa kibali na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”