Luka 1:11-20
Luka 1:11-20 NENO
Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zakaria. Zakaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu. Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina Yahya. Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Mwenyezi Mungu, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu wa Mungu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Naye atawageuza wengi wa Waisraeli warudi kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Naye atatangulia mbele za Mwenyezi Mungu katika roho na nguvu ya Ilya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuwaweka tayari watu walioandaliwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.” Zakaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.” Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Jibraili, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”