Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 21

21
Sheria kwa ajili ya makuhani
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na makuhani, wana wa Haruni, uwaambie: ‘Kamwe kuhani asijitie unajisi kwa ajili ya mtu wake yeyote anayekufa, 2isipokuwa jamaa wake wa karibu, kama vile mama yake au baba yake, mwanawe au binti yake, ndugu yake, 3au dada yake asiyeolewa ambaye anamtegemea kwa kuwa hana mume, kwa ajili ya hao aweza kujitia unajisi. 4Kamwe asijitie unajisi mwenyewe kutokana na wale watu ambao anahusiana nao kwa kuoana, na hivyo kujitia unajisi.
5“ ‘Kamwe makuhani wasinyoe nywele za vichwa vyao wala wasinyoe pembeni mwa ndevu zao, au kuweka chale kwenye miili yao. 6Lazima wawe watakatifu kwa Mungu wao, na kamwe wasilinajisi jina la Mungu wao. Kwa sababu ndio wanaotoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu, chakula cha Mungu wao, hivyo lazima wawe watakatifu.
7“ ‘Kamwe wasioe wanawake waliojinajisi kwa ukahaba, au waliopewa talaka na waume wao, kwa sababu makuhani ni watakatifu kwa Mungu wao. 8Waoneni kuwa watakatifu, kwa sababu ndio wanaotoa chakula cha Mungu wenu. Kumbukeni kuwa ni watakatifu, kwa sababu Mimi Mwenyezi Mungu ni mtakatifu, Mimi niwafanyaye ninyi kuwa watakatifu.
9“ ‘Ikiwa binti ya kuhani anajitia unajisi kwa kufanya ukahaba, anamwaibisha baba yake; lazima achomwe kwa moto.
10“ ‘Kuhani mkuu, yule miongoni mwa ndugu zake ambaye amekwisha kupakwa mafuta kwa kumiminiwa juu ya kichwa chake, na ambaye amewekwa wakfu kuvaa mavazi ya ukuhani, kamwe asiache nywele zake bila kufunikwa, wala asirarue nguo zake. 11Kamwe asiingie mahali palipo maiti ndani. Kamwe asijitie unajisi, hata kwa ajili ya baba yake au mama yake, 12wala asiondoke mahali patakatifu pa Mungu wake au kupanajisi, kwa sababu amewekwa wakfu kwa mafuta ya Mungu wake. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
13“ ‘Mwanamke atakayeolewa na kuhani lazima awe bikira. 14Kamwe asimwoe mjane, au mwanamke aliyepewa talaka, wala mwanamke aliyejinajisi kwa ukahaba, bali atamwoa tu bikira kutoka miongoni mwa watu wake, 15na hivyo hatawatia unajisi wazao wake miongoni mwa watu wake. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nimfanyaye mtakatifu.’ ”
16Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 17“Mwambie Haruni: ‘Kwa vizazi vijavyo, hakuna mzao wako mwenye dosari atakayekaribia kutoa chakula cha Mungu wake. 18Hakuna mtu mwenye dosari yoyote awezaye kukaribia: hakuna mtu aliye kipofu au kiwete, au aliyeharibika uso au asiye na viungo kamili, 19hakuna mtu mwenye mguu au mkono uliolemaa, 20au mwenye kibiongo au aliyedumaa, au aliye na tatizo la macho, au aliye na uvimbe wenye usaha au majipu, au aliyehasiwa. 21Hakuna mzao wa kuhani Haruni mwenye kilema chochote atakayekaribia kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. Kama ana kilema, kamwe asikaribie kutoa chakula cha Mungu wake. 22Anaweza kula chakula kitakatifu sana cha Mungu wake, pia hata chakula kitakatifu. 23Lakini kwa sababu ya kilema chake, kamwe asikaribie pazia wala kukaribia madhabahu, asije akanajisi mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwafanyaye watakatifu.’ ”
24Basi Musa akanena na Haruni, na wanawe, na Waisraeli wote.

Iliyochaguliwa sasa

Walawi 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia