Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 5

5
1Basi wafalme wote wa Waamori magharibi mwa Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri tena wa kukabiliana na Waisraeli.
Tohara huko Gilgali
2Wakati huo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya gumegume na uwatahiri Waisraeli tena.” 3Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya gumegume na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi#5:3 maana yake Kilima cha magovi.
4Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. 5Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini kutoka Misri hawakuwa wametahiriwa. 6Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini hadi wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Mwenyezi Mungu. Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. 7Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. 8Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini hadi walipopona.
9Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.
10Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa wamepiga kambi huko Gilgali kwenye nchi tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. 11Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi: mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. 12Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
Jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu
13Basi Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”
14Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu.” Yoshua akasujudu, uso wake ukigusa chini, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” 15Jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali uliposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.

Iliyochaguliwa sasa

Yoshua 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia