Yoshua 22:1-9
Yoshua 22:1-9 NEN
Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Mose mtumishi wa BWANA aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi BWANA Mungu wenu aliyowapa. Sasa kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ile ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwapa ngʼambo ya Yordani. Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa BWANA alizowapa: yaani kumpenda BWANA Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.” Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani mwao. (Kwa nusu ya kabila la Manase Mose alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi ya Yordani pamoja na ndugu zao). Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki, akisema, “Rudini nyumbani mwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia wingi wa nguo, nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.” Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la BWANA kupitia Mose.