Ayubu 34:16-30
Ayubu 34:16-30 NEN
“Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili; sikilizeni hili nisemalo. Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala? Je, utamhukumu mwenye haki, Aliye na Nguvu Zote? Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’ nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’ yeye asiyependelea wakuu, wala haonyeshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake? Wanakufa ghafula, usiku wa manane; watu wanatikiswa nao hupita; wenye nguvu huondolewa bila mkono wa mwanadamu. “Macho yake yanazitazama njia za wanadamu; anaona kila hatua yao. Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa, ambapo watenda mabaya wanaweza kujificha. Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana, ili apate kuja mbele zake kwa hukumu. Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote, huwaondoa usiku, nao wakaangamia. Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona, kwa sababu wameacha kumfuata Mungu, nao hawakuiheshimu njia yake hata moja. Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake, hivyo akasikia kilio cha wahitaji. Lakini kama akinyamaza kimya, ni nani awezaye kumhukumu? Kama akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumwona? Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa, ili kumzuia mtu mwovu kutawala, au wale ambao huwategea watu mitego.