Ayubu 15
15
Elifazi anasema: Ayubu anadhoofisha imani
1Kisha Elifazi Mtemani akajibu:
2“Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu,
au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki?
3Je, aweza kubishana kwa maneno yasiyofaa,
kwa hotuba zisizo na maana?
4Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu
na kuzuia ibada mbele za Mungu.
5Dhambi yako inasukuma kinywa chako,
nawe umechagua ulimi wa hila.
6Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu;
midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako.
7“Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?
Ulizaliwa kabla ya vilima?
8Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu?
Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe?
9Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi?
Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?
10Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu,
watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako.
11Je, faraja za Mungu hazikutoshi,
au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu?
12Kwa nini moyo wako unakudanganya,
na kwa nini macho yako yanang’aa,
13ili upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu,
na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako?
14“Mwanadamu ni kitu gani,
hata aweze kuwa safi,
au yeye aliyezaliwa na mwanamke,
hata aweze kuwa mwadilifu?
15Kama Mungu hawaamini watakatifu wake,
kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake,
16sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu,
ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!
17“Nisikilize mimi nami nitakueleza,
acha nikuambie yale niliyoyaona,
18ambayo watu wenye hekima wameyanena,
bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao
19(wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi,
hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):
20Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso,
miaka yote aliwekewa mkorofi.
21Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake;
katika kufanikiwa kwake, wanyang’anyi humshambulia.
22Hukata tamaa kuokoka gizani;
amewekwa kwa ajili ya upanga.
23Hutangatanga, akitafuta chakula;
anajua kwamba siku ya giza iko karibu.
24Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu;
humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,
25kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake
na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,
26kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu
akiwa na ngao nene, iliyo imara.
27“Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene
na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,
28ataishi katika miji ya magofu,
na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote,
nyumba zinazokuwa vifusi.
29Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu,
wala mali yake haitakuwa nyingi juu ya nchi.
30Hatatoka gizani;
mwali wa moto utanyausha machipukizi yake,
nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.
31Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili,
kwa kuwa hatapata malipo yoyote.
32Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake,
nayo matawi yake hayatastawi.
33Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva,
kama mzeituni unaodondosha maua yake.
34Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa,
nao moto utateketeza mahema ya wale wanaopenda rushwa.
35Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu;
tumbo zao huumba udanganyifu.”
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 15: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.