Yohana 9:13-23
Yohana 9:13-23 NEN
Wakamleta kwa Mafarisayo yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali. Basi siku hiyo Yesu alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato. Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.” Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika. Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho, wasemaje kuhusu mtu huyo?” Maana macho yako ndiyo yaliyofumbuliwa. Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.” Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake. Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. Lakini sisi hatujui ni kwa jinsi gani kwamba sasa anaona, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni, yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Yesu kuwa ndiye Kristo atafukuzwa kutoka sinagogi. Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”