Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 9:1-12

Yohana 9:1-12 NEN

Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.” Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona. Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?” Wengine wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.” Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.” Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?” Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!” Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?” Akawajibu, “Sijui.”