Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 8:37-59

Yohana 8:37-59 NENO

Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Ibrahimu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. Ninasema yale niliyoyaona nikiwa mbele za Baba yangu, nanyi mnafanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.” Wakajibu, “Baba yetu ni Ibrahimu.” Isa akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Ibrahimu, mngefanya mambo yale aliyofanya Ibrahimu. Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya jambo la namna hii. Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.” Isa akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. Ninyi ni watoto wa baba yenu, ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli, maana hamna kweli ndani yake. Anaposema uongo, yeye husema lugha yake ya asili kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. Lakini kwa sababu nimewaambia kweli, hamkuniamini! Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.” Wayahudi wakamjibu Isa, “Je, hatuko sahihi tunaposema kwamba wewe ni Msamaria, na kwamba una pepo mchafu?” Isa akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau. Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi. Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu, hataona mauti milele.” Ndipo Wayahudi wakapaza sauti, wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu! Ibrahimu alikufa, na manabii vilevile, nawe unasema kuwa mtu akitii neno lako hatakufa milele. Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu ambaye alikufa, na manabii ambao pia walikufa? Unafikiri wewe ni nani?” Isa akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi. Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake. Baba yenu Ibrahimu alishangilia kwamba angeiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.” Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, nawe wasema umemwona Ibrahimu?” Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Ibrahimu hajakuwa, Mimi niko.” Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Isa akajificha, naye akatoka Hekaluni.