Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 8:21-36

Yohana 8:21-36 NENO

Isa akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kuja.” Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?” Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini; mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu. Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu; kwa maana msipoamini kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani?” Naye Isa akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo. Nina mambo mengi ya kusema kuwahusu ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kuaminika, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.” Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia kuhusu Baba yake wa Mbinguni. Kisha Isa akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua Mwana wa Adamu juu, ndipo mtajua kuwa mimi ndiye yule niliyesema, na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu, bali ninasema yale tu Baba yangu amenifundisha. Yeye aliyenituma yu pamoja nami; hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.” Wengi waliomsikia Isa akisema maneno haya wakamwamini. Kisha Isa akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.” Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Ibrahimu, nasi hatujakuwa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” Isa akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.