Yohana 6:60-71
Yohana 6:60-71 NENO
Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?” Isa alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Isa alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata. Hivyo Isa akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.” Ndipo Isa akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” (Hapa alikuwa anasema kuhusu Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Isa.)