Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 5:25-47

Yohana 5:25-47 NENO

Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai. Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu. “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake, nao watatoka makaburini. Wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima, nao wale waliotenda maovu watafufuka ili wahukumiwe. “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Lakini yuko mwingine anishuhudiaye, na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli. “Mlituma wajumbe kwa Yahya, naye akaishuhudia kweli. Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu; la, bali ninalitaja hili ili ninyi mpate kuokolewa. Yahya alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake. “Ninao ushuhuda mkuu kuliko ule wa Yahya. Kazi ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, kazi hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba amenituma. Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele. Maandiko haya ndio yanayonishuhudia mimi. Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima. “Mimi sikubali kutukuzwa na wanadamu, lakini mimi ninawafahamu. Ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei. Lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. Mnawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamfanyi bidii kupata utukufu unaotoka kwa Mungu? “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba. Mshtaki wenu ni Musa, ambaye mmemwekea tumaini lenu. Kama mngemwamini Musa, mngeniamini na mimi, kwa maana aliandika habari zangu. Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Musa, mtaaminije ninayoyasema?”