Yohana 4:4-30
Yohana 4:4-30 NENO
Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. Kisima cha Yakobo kilikuwa huko. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.) Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.) Isa akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.” Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?” Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.” Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisije tena hapa kuteka maji!” Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano, na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.” Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.” Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini: wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba anawatafuta watu wanaomwabudu kwa namna hii. Mungu ni Roho, na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Al-Masihi” (yaani Aliyetiwa mafuta) “anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.” Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.” Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au, “Kwa nini unazungumza naye?” Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini, akawaambia watu, “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Al-Masihi?” Basi wakamiminika watu kutoka mjini, wakamwendea Isa.