Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19:23-30

Yohana 19:23-30 NEN

Askari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini. Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari. Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake. Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 19:23-30