Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 18:28-37

Yohana 18:28-37 NEN

Ndipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka. Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?” Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.” Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.” Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia. Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Yesu, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?” Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?” Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.” Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 18:28-37