Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 18:19-40

Yohana 18:19-40 NENO

Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Isa kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake. Isa akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale waliosikia yale niliyowaambia. Wanajua niliyoyasema.” Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye akampiga Isa kofi usoni. Kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Isa akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” Ndipo Anasi akampeleka Isa kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa. Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya watu waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?” Petro akakana, akasema, “Sio mimi.” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Isa?” Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo. Ndipo viongozi wa Wayahudi wakamchukua Isa kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala Mrumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri. Ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani ya jumba kwa sababu walitaka kushiriki katika Pasaka. Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa, akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?” Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu, tusingemleta kwako.” Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.” Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Isa kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia. Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Isa, akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Isa akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu?” Pilato akamjibu, “Je, mimi ni Myahudi? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?” Isa akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa viongozi wa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.” Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Isa akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni: ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.” Pilato akamuuliza Isa, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena, akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Isa, “Sioni msingi wowote wa kumshtaki mtu huyu. Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘mfalme wa Wayahudi’?” Wao wakapiga kelele, wakajibu, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyang’anyi.