Yohana 18:1-18
Yohana 18:1-18 NENO
Isa alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake, wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani; yeye na wanafunzi wake wakaingia humo. Basi Yuda, aliyemsaliti, alipafahamu mahali hapo, kwani Isa alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. Hivyo Yuda akaja kwenye bustani akiongoza kikosi cha askari Warumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha. Isa, akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao, akawauliza, “Mnamtafuta nani?” Wao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.” Isa akawajibu, “Mimi ndiye.” (Yuda, aliyemsaliti, alikuwa amesimama pamoja nao.) Isa alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini! Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.” Isa akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.” Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. (Mtumishi huyo aliitwa Malko.) Isa akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?” Hivyo wale askari, wakiwa na jemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Isa na kumfunga. Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule. Kayafa ndiye alikuwa amewashauri viongozi wa Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu. Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Isa. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia uani kwa kuhani mkuu pamoja na Isa. Lakini Petro alisimama nje karibu na lango. Ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani. Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akajibu, “Sio mimi.” Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.