Yohana 16:16-24
Yohana 16:16-24 NENO
Isa akaendelea kusema, “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.” Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’? Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninaenda kwa Baba’?” Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo’? Hatuelewi hilo analosema.” Isa akatambua kuwa walitaka kumuuliza kuhusu hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’? Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke anapokuwa na uchungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha yake ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia, mkimwomba Baba jambo lolote kwa jina langu, yeye atawapa. Hadi sasa hamjaomba jambo lolote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.