Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 14:1-11

Yohana 14:1-11 NENO

Isa akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mnamwamini Mungu, mniamini pia. Nyumbani mwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningewaambia. Naenda kuwaandalia makao. Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo nanyi mpate kuwepo. Ninyi mnajua njia ya kufika ninakoenda.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakoenda, tutaijuaje njia?” Isa akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kupitia kwangu. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, na hiyo itatutosha.” Isa akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuoneshe Baba’? Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba, na Baba yuko ndani yangu; la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.