Yohana 11:47-57
Yohana 11:47-57 NENO
Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa Baraza la Wayahudi. Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi. Tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.” Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote! Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?” Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe, bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Isa angekufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi; wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja. Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Isa. Kwa hiyo Isa akawa hatembei tena hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake. Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu ili wakajitakase kabla ya Pasaka. Watu wakawa wanamtafuta Isa, nao waliposimama kwenye ua la Hekalu, waliulizana, “Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?” Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Isa aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.