Yohana 10:7-21
Yohana 10:7-21 NEN
Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.” Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika. Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.” Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”