Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 10:1-17

Yohana 10:1-17 NENO

“Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang’anyi. Yeye anayeingia kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. Mlinzi humfungulia lango, na kondoo huisikia sauti yake. Yeye huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. Baada ya kuwatoa wote nje, yeye hutangulia mbele yao na kondoo humfuata, kwa kuwa wanaijua sauti yake. Lakini kondoo hawatamfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” Isa alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia. Kwa hiyo Isa akasema nao tena, akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. Wote walionitangulia ni wezi na wanyang’anyi, nao kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi lango. Yeyote anayeingia zizini kupitia kwangu ataokoka. Ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwizi huja ili aibe, aue na aangamize. Mimi nimekuja ili wapate uzima, kisha wawe nao tele. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Anapomwona mbwa-mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa-mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu, nao kondoo wangu wananijua. Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, ndivyo nami ninautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili. Inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu; hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.